Rais wa El Salvador ametangaza kukamatwa kwa shehena kubwa zaidi ya dawa za kulevya katika historia ya nchi hiyo baada ya Jeshi la Wanamaji kuiteka meli ya usambazaji wa baharini FMS Eagle yenye uzito wa tani 1,200 (DWT), takribani kilomita 700 kutoka pwani ya El Salvador.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Rais Bukele, meli hiyo iliyokuwa ikipeperusha bendera ya Tanzania ilikutwa na tani 6.6 za kokaini zilizofichwa ndani ya matangi ya ballast kwa kutumia vyumba vya siri. Dawa hizo zinakadiriwa kuwa na thamani ya karibu dola za Marekani milioni 165, hatua aliyoitaja Rais Bukele kama “pigo kubwa na la kihistoria dhidi ya mitandao ya biashara ya dawa za kulevya.”
Wakati wa operesheni hiyo, wafanyakazi 10 wa meli walikamatwa wakiwemo raia nne wa Colombia, watatu wa Nicaragua, wawili wa Panama na mmoja wa Ecuador. Video iliyotolewa na serikali inaonesha wapiga mbizi maalum wakikagua na kutoa vifurushi vya dawa kutoka ndani ya meli.
Meli ya FMS Eagle iliripotiwa kuwa nje ya mfumo wa AIS kwa zaidi ya siku 12, huku hifadhidata ya Equasis ikionesha taarifa zisizo wazi kuhusu bendera yake na ikidokeza kuwa inamilikiwa na kuendeshwa kutoka Marekani. Hakuna kumbukumbu za ukaguzi wa usalama wa bandari (PSC) kwa meli hiyo.
Tukio hili linajiri wiki chache baada ya operesheni nyingine kubwa katika Bahari ya Pasifiki Kusini, ambako karibu tani tano za kokaini zilikamatwa katika meli iliyokuwa ikielekea Australia, operesheni iliyosifiwa na Australian Federal Police na Australian Border Force. Hadi sasa, haijaelezwa wazi dawa hizo zilitoka wapi wala zilikuwa zikielekea wapi, wakati watuhumiwa wakitarajiwa kufikishwa mahakamani. Serikali ya El Salvador imesisitiza itaendelea na operesheni kali dhidi ya uhalifu wa kimataifa wa dawa za kulevya. © Copyright
No Comments Yet...